Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wananchi wa kaunti ya Nyamira ambao wamekuwa wakipata ugumu wakutumia barabara mbovu sasa wamepata sababu yakutabasamu baada ya serikali ya kaunti hiyo kununua magari manne aina ya tipper, manne aina ya pickup, moja aina ya toyota prado itakayo tumiwa na spika na tingatinga mbili zitakazotumika kukarabati barabara za kaunti hiyo.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa magari hayo siku ya Jumanne, mkuu wa muda wa barabara na miundomisingi Bi Janet Komenda alisema kwamba kutokana na ununuzi wa magari hayo, idara yake itafanya juhudi kuhakikisha kwamba barabara mpya zinafunguliwa na pia kuhakisha kwamba zingine zinakarabatiwa.

"Kutokana na ununuzi wa magari mpya yakujenga na kukarabati barabara kwenye kaunti hii, naahidi kwamba idara yangu itafanya juhudi kuhakikisha kuwa barabara mpya zinafunguliwa huku zingine zikikarabatiwa,” alisema Komenda.

Komenda alisema idara yake imeweka mikakati kabambe kuhakikisha kwamba kwa miezi mitatu ijayo, gari lakuzima moto litakuwa limenunuliwa ili kuthibiti visa vya moto vinavyoshuhudiwa mara kwa mara.

Komenda vilevile amewaomba wawakilishi wadi kutoingilia ratiba ya utendakazi wa idara yake huku akiwasihi kungoja idara hiyo kufika kwenye wadi zao ili kurekebisha barabara.

"Nawaomba wawakilishi wadi kutoingilia ratiba ya utendakazi wa idara hii, ila nawasihi wangoje maafisa wakukarabati barabara kufika katika maeneo yao,” alisema Komenda.

Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama amewaonya maafisa wa idara hiyo ya barabara na miundomisingi dhidi yakutumia magari hayo kwa shughuli zao za kibinafsi akisema kwamba watachukuliwa hatua kali.

"Afisa yeyote wa idara ya barabara na miundomisingi atakaye patikana akitumia magari haya kwa shughuli zao za kibinafsi awe tayari kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu,” alisema Nyagarama.

Nyagarama aidha amewasihi wananchi kuripoti visa vyovyote vya utumizi mbaya ma magari ya umma huku akiwasihi maafisa wa idara hiyo kuwajibikia kazi zao.