Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu mkuu wa chama cha kutetea walimu cha Knut katika kaunti ya Mombasa tawi la Kilindini, Bwana Dan Oloo, ameshtumu serikali kwa kuratibu tarehe ya kufanya mtihani.

Oloo ameitaka Wizara ya Elimu kusongeza tarehe hiyo mbele huku suala la mgomo wa walimu likiafutiwa suluhu.

Akiongea na waandishi wa habari katika afisi yake siku ya Jumanne, Oloo alisema kuwa si vyema kuweka tarehe ilhali walimu bado wanaendelea na mgomo.

Alisema kuwa wanafunzi hawatakuwa na ukakamavu wa kufanya mitihani hiyo kwa sababu tayari washaathiriwa na mgomo huo na wameweza kupoteza muda mwingi.

Oloo alisema serikali ya Jubilee imefanya kinyume na maagano wakati walikuwa wakifanya kampeni za kutafuta kura, ambapo waliahidi kuwa watapigania haki za wafanyakazi wa umma ambapo walimu ni wamoja wao.

“Tayari serikali inaonekana kutojali masilahi ya wanafunzi wa Kenya na ingekuwa vizuri zaidi tarehe ya mtihani wa kitaifa katika darasa la nane na kidato cha nne kusongezwa mbele kidogo hadi mgomo wa walimu utatuliwe,” alisema Oloo.

Aliitaka Wizara ya Elimu, pamoja na tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC kutafuta mwafaka wa kudumu katika kulishughulikia suala hilo ambalo tayari limesambaratisha shughuli za elimu katika kaunti zote nchini.

Alishangaa ni kwa nini viongozi wa serikali wanaendelea kusema kuwa hawana pesa za kuwaongeza walimu mishahara ilhali walimu hao huchangia ukuaji wa uchumi nchini kwa kulipa ushuru.