Abiria katika kituo cha magari mjini Kisii wamelalamikia wizi ambao unaendelea kutekelezwa katika kituo hicho na watu wasiojulikana.
Wakiongea siku ya Alhamisi katika kituo hicho mjini Kisii, abiria hao waliomba serikali kuweka maafisa wa usalama katika vituo vya magari hasa hicho kilichoko mjini Kisii ili wizi wa aina hiyo uweze kupungua.
Marta Ondigi, abiria aliyenusurika kuibiwa alisema kuwa begi aliyoibeba ilikuwa na simu pamoja na pesa alizokuwa ametoa kwa benki ili apeleke mwanawe shuleni juma lijalo.
Ondigi alisema kuwa alinisurika baada ya juhudi za mwizi huyo kugonga mwamba. Mwizi huyo alipata kichapo kutoka kwa madereva wa kituo hicho baada ya kumfumania akitaka kutekeleza wizi huo.
“Sisi hatujui mwizi huyo alikotoka wapi. Alikuwa na nia ya kumuibia mama huyu aliyekuwa na karo ya mtoto wake lakini kwa bahati nzuri, alishambuliwa na madereva,” alisema Charles Nyaanga, dereva wa magari ya kuelekea Marani.
“Tunaomba serikali kuu pamoja na ile ya kaunti kutuwekea usalama kwa kuajiri maafisa wa polisi ambao watakuwa wanalinda kituo hiki ili kukomesha wizi,” alisema Jane Obebo, abiria.
Visa vya wizi vimekuwa vikishuhudiwa katika kituo hicho, jambo ambalo limewapelekea abiria kuomba serikali kuingilia kati ili kuimarisha usalama mjini kisii hasa katika vituo vya magari.