Wakaazi wa kaunti ya Kisii wameiomba serikali kuwajengea uwanja wa kupumzikia [city park] baada ya kumaliza kufanya kazi.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, wakaazi hao wakiongonzwa na Phillip Omwancha walisema serikali ya kaunti ya kisii inastahili kutafuta mahala pa kujenga uwanja ambao utatumika kwa mapumziko kama mji mingine mikuu humu nchini.
“Tunaomba serikali iweke mikakati ya kuanzisha uwanja huo hapa ili watu wawe wanapumzika baada ya kazi kama miji mingine mikuu,” alisema Hellen Oribo, mkaazi.
Wakati huo huo, wakaazi hao walisema tayari serikali ya kaunti hiyo iko na uwanja ambao unaitwa Erera, kilomita moja kutoka mji wa Kisii na kutaka uwanja huo utumike kwa shugli hiyo na kukarabatiwa kikamilifu.
“Serikali ikifanya hivyo tutashukuru sana maana kama mimi huwa namaliza kazi saa nane mchana, na ninashindwa kuenda kwa nyumba saa hizo, tungekuwa na uwanja wa mapumziko kama Nairobi City Park, ama Uhuru Park, mahala watu wanapumzikia itakuwa vyema zaidi,” alihoji Brian Osiemo, mkaazi.
Sasa ni jukumu la serikali ya kaunti ya Kisii kusikia ombi la wakaazi hao kutenga na kujenga uwanja huo kama njia moja ya kuimarisha mazingira mema kwa watu wa kaunti nzima ya kisii.