Wakimbizi wa ndani kutoka Wadi ya Esise, Eneo Bunge la Borabu wameomba serikali kuwafadhili pesa zao ili waweze kujiendeleza.
Wito huo umetolewa baada ya wakimbizi hao kukosa kulipwa kwa miaka saba iliyopita jambo ambalo wameshangazwa nalo na kuomba serikali kuwakumbuka kama waathiriwa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika wadi hiyo, mwenyekiti wa wakambizi katika eneo hilo, Ayubu Nyambati alisema tangu waathirike kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 na 2008 bado hawajafadhiliwa.
Mwenyekiti huyo aliomba serikali ya kitaifa kuwalipa kama wakimbizi wengine kwani wengi wao walipoteza mali yao na kusababishiwa hasara kubwa.
“Tulipoteza mali mingi na tulichomewa nyumba zetu tukapata hasara kubwa. Huwa tunasikia wakimbizi katika sehemu zingine walifadhiliwa lakini sisi hapa Esise hatujafadhiliwa. Tunaomba serikali itukumbuke kama ilivyokumbuka wathiriwa wengine katika sehemu zingine hapa nchini,” alisema Nyambati.
Wakimbizi hao ambao hawajafadhiliwa hadi sasa ni wale ambao walikuwa mpakani Borabu Bomet
Nyambati alisema kuwa bado wana matumaini kuwa watapata haki yao.