Wazazi kutoka kaunti ya Kisii wameiomba serikali kuu na tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC kuwashughulikia walimu kikamilifu ili kuzuia mgomo ambao unapangwa kuanza katika muhula huu kama matakwa yao hayataafikiwa jinsi mahakama ilivyoagiza.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, mjini Kisii, wakati wengi wao walikuwa wakiwapeleka wanao shuleni, wazazi hao, Beatrice Orina, Vincent Obiri na wengine walikuwa na hofu kuwa wanaweza peleka wanao shuleni na wapate walimu wameanza mgomo.
wazazi hao walisema kuwa walimu wakigoma hasa katika muhula huu wa tatu, wanafunzi ndio hukumbwa na shida kubwa kwa sababu muhula huu ndio mitihani wa kitaifa huandaliwa ambayo hutayarisha maisha ya siku sijazo kwa watoto.
Beatrice Orina alisema kuwa walimu wanastahilii kushughulikiwa kwani wanafanya kazi ngumu na njia ya kuzuia migomo hiyo ni kushirikiana na kupata suluhu la kudumu katika Sekta ya Elimu.
“kwa upande wangu naomba serikali yetu na tume ya kuwaajiri walimu kuwashughulikia walimu na kuelewana nao ili mambo ya mgomo ambayo hutuumiza sisi kama wazazi na watoto wetu yakomeshwe,” alisema Orina.
Wakati walimu wanagoma mara nyingi viwango vya masomo hupungua kwa asilimia kubwa na wanafunzi huwa na changamoto nyingi kupita kiasi haswa wanaofanya mitihani wa kitaifa,” alisema Vincent Obiri.