Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeombwa kuwapa ajira vijana waliowacha pombe ili kuwazuia kujihusisha na mambo ya uhalifu.

Wito huo umetolewa baada ya vijana ambao walikuwa wakibugia pombe hapo awali kuonekana wakizurura bila kazi na kushukiwa huenda waanze kutekeleza uhalifu.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika wadi ya Rigoma, eneo bunge la Kitutu Masaba, wakazi wa wadi hiyo, wakiongozwa na Victor Onchiri, walisema wanahofia vijana hao wataanza kuwaibia mali yao kwani hapo awali pombe ilikuwa inawazuia kutotekeleza wizi.

Haya yanajiri baada ya ng’ombe mmoja kuibwa kutoka zizi la mkazi mmoja wa eneo hilo lakini kwa bahati nzuri, ng’ombe huyo alipatikana amefungwa kilomita moja kutoka kwa mkazi huyo.

Kulingana na wakazi hao, pombe ilikuwa inawatuliza vijana huku wakisema wakati huu vijana hao hawana kazi na kusalia kuzembea na kurandaranda jambo ambalo wameshuku huenda likawasababisha kutekeleza wizi.

“Ikiwa serikali ya kaunti inahitaji kutusaidia, tunaomba itafutie vijana hawa ambao wamekuwa wakibugia pombe ajira, hata kama ni ya kufagia masoko bora wasikae nyumbani kuzembea,” alisema David Makworo, mkazi.

“kama vijana hawa hawana kazi ya kufanya, wataanza kutuibia mali zetu hapa nyumbani na wakifumaniwa watauawa,” alisema Joyce Omariba, mkazi.

Hata hivyo, wakazi hao walipongeza maafisa wa polisi kwa kukomeza kupikwa kwa pombe haramu.