Baadhi ya Wawakilishi wa wadi mbalimbali katika Kaunti ya Nyamira siku ya Alhamisi walidai kuna baadhi ya watoza ushuru wanao risiti bandia wanayotumia kujipatia pesa, bali sio ya serikali ya kaunti hiyo.
Wawakilishi hao walidai kuwa serikali ya Kaunti ya Nyamira imekuwa ikipoteza pesa nyingi baada ya kubainika kuwa watoza ushuru wa kaunti hiyo wana ujanja kwani wanadaiwa kuwa na vitabu vya risiti viwili; kile cha serikali na kile cha kibinafsi ambacho wamejitengenezea wao wenyewe huku wakikitumia kujipatia pesa zao badala ya kutumia kile cha serikali kutengenezea serikali pesa kupitia ushuru.
Madai haya yalifikishwa katika bunge la kaunti hiyo siku ya Alhamisi na Mwakilishi mteule Fred Menge aliyesema alijionea mwenyewe huku mwenzake Mwakilishi Naumi Ondieki akimuunga mkono na kusema ni ukweli baadha ya watoza ushuru wa soko mbalimbali katika Kaunti ya Nyamira wana vitabu vya risiti viwili huku wakitumia kile cha kibinafsi kujipatia pesa badala ya kutengenezea serikali pesa.
“Wanao jukumu la kutoza ushuru wana vitabu viwili ndio maana serikali yetu haipati pesa vizuri maana hawatumii kile kitabu cha serikali wakati mwingi, bali wanakitumia kile chao kujinufaisha wao wenyewe,” alidai Mwakilishi Menge.
Wakati uo huo, Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alimwagiza mwenyekiti wa kamati ya pesa katika bunge hilo Alfayo Ongeresa kuzunguka katika soko mbalimbali kufanya uchungunzi kuhusiana na madai hayo.
Mwenyekiti huyo aliitikia agizo la spika na kusema atafanya uchunguzi na kufikisha ripoti kamili katika bunge hilo ndani ya wiki moja ili ukweli halisi wa mambo ubainike.