Serikali imetakiwa kuharakisha ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu ili kupunguza msongamano wa abiria na magari unaoshuhudiwa katika kivuko cha Feri.
Baadhi ya wenye magari wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumapili walieleza kuwa imekuwa kero kutumia kivuko hicho kwa muda sasa kutokana na msongamano mkubwa wa magari na abiria, na kuongeza kuwa huduma za shirika hilo haziridhishi kamwe kutokana na kushuhudiwa kuharibika mara kwa mara kwa feri hizo.
Hamisi Salim, mmoja wa dereva wa gari alieleza kuwa uchelewa kazini kila wakati kutokana na msongamano uliopo katika kivuko hicho.
Aidha, aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, kivuko hicho kimekuwa hatari kwa watoto na watu wasiojiweza wakati kunapokuwa na msukumano.
Wakati huo huo, shirika la huduma kwa feri limeeleza kwamba msongamano wa abiria na magari ulioko sasa unasababishwa na kuondolewa kwa baadhi ya feri kwa ajili ya marekebisho.
Shirika hilo limeeleza kwamba kwa sasa feri mbili tu ndio zitatoa huduma hadi pale feri tatu nyengine zitakapofanyiwa marekebisho ya kimitambo.
Mkuu wa idara ya uhusiano mwema wa shirika hilo Elizabeth Washira alisema siku ya Ijuma kuwa feri zinazorekebishwa ni M.V Harambee, M.V Nyayo na M.V Kilindini.
Feri zinazotoa huduma kwa sasa ni M.V Likoni na M.V Kwale, ambapo moja wapo haiwezi kubeba magari kwa sababu ya mlango mbovu.
Kuanzia siku ya Alhamisi, abiria katika kivuko hicho wamekuwa wakilalamikia huduma duni, huku wengine wakijeruhiwa katika msongamano wa watu.