Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya Japani kupitia kwa shirika lisilo la kiserikali la Community Roads Enterprise (CORE) itaanzisha ujenzi na ukarabati wa barabara kupitia technolojia mpya inayojulikana kama DO-NOU.

Akiongea siku ya Ijumaa katika taasisi ya Kenya Institute of Highway and Building Technology ilioko katika mji wa Kisii, Naibu balozi wa Japani Nchini, Bwana Mikio Mori, alisema kuwa serikali ya Japani imetenga kiwango kikubwa cha hela ili kuboresha na kuimarisha barabara hasa zile za vijijini.

Mori alisema kuwa teknolojia hiyo ya DO-NOU ambayo imetolewa kwajina la kijapani hutumia mchanga thabiti kwenye vibebezi na kuzamishwa kwenye maeneo ambayo mara nyingi huwa na chemichemi za maji na kufanya barabara kuwa imara na thabiti hata zaidi ya miaka saba.

"Tunalenga kuanza na barabara za mjini Kisii ambazo huwa hazipitiki mara kwa mara. Vijana waliofuzu kutoka Kaunti za Kisii na Nyamira watasaidia kufanikisha mradi huo kwa ushirikiano na shirika la CORE," alisema Mori.

Naibu balozi huyo aliishukuru serikali ya Kaunti ya Kisii na serikali kuu kwa kuwapa nafasi kama wawekezaji kutoka Japani kwa kuanzisha miradi ya kuboresha miundomisingi kwa kushirikisha wananchi wa kawaida.