Shirika la Jubilee Insurance katika kaunti ya Kisii limewanunulia baadhi ya wakaazi 7,300 wa kaunti hiyo kadi za matibabu al maarufu NHIF.
Mweyekiti wa chama cha Receivable Performance Management (RPM) Credit kaunti ya Kisii Lumumba Nyaberi alithibitisha haya baada ya wakaazi hao kupokea mikopo ya pesa kutoka chama cha Vision Fund na chama hicho cha RPM Crediti kwa takribani miezi saba zilizopita.
Akizungumza na Waandishi wa habari siku ya Jumapili katika mji wa Kisii, mwenyekiti Nyaberi alisema kuwa shirika hilo liliamua kufanya hivyo ili pesa zile wakaazi hao watazipata kama mikopo wafanyie biashara na sio kupambana na kutibu ugonjwa tu pindi familia zao zinapougua.
Ikumbukwe kuwa shirika la Jubilee Insurance ndilo linasimamia chama cha Vision Fund na RPM Credit katika kaunti ya Kisii.
"Wale watu tumekabidhi mikopo wamenunuliwa kadi za matibabu ili wawe wanazitumia wakati wanapougua kama njia moja wapo ya kuwazuia kutumia pesa zile tumewapa kama mikopo kufanyia bishara na kupunguza hali ya umaskini katika kaunti hii ya Kisii," alihoji Nyaberi, mwenyekiti wa chama cha RPM Credit.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kadi hizo za matibabu ambazo watu hao walipokezwa ziligharamia matibabu hadi Sh200,000 kwa mwaka mmoja.
"Yeyote ambaye amechukua mkopo kutoka chama cha RPM na Vision fund amenunuliwa kadi ya matibabu yenye inasimamia matibabu yao watakapo kuwa wagonjwa," aliongeza Nyaberi.