Share news tips with us here at Hivisasa

Hata baada ya serikali kuu kufunga shule zote za umma na zile za binafsi siku ya Ijumaa, agizo hilo bado linaendelea kupingwa na wengi wa walimu wa shule za kibinafsi, huku ikionyesha kuwa nyingi ya shule hizo zimekuwa masomoni kama kawaida.

Katika uchunguzi uliofanya siku ya Jumatatu asubuhi, nyingi ya shule hizo zimepokea wanafunzi wao na masomo yanaendelea vizuri, huku nyingi ya shule za umma katika kaunti ya Kisii zikiwa hazina wanafunzi wala walimu ila wafanyakazi kama askari na wahudumu wengine.

Mmoja wa walimu wa shule za Kimataifa za Bridge International Bwana Fred Omwoyo,  shule za binafsi zinajisimamia na si haki serikali kuamua tu kuwa shule zifungwe bila hata kushauriana na washika dau wa sekta ya elimu.

Aidha, alimtaka kiongozi wa nchi, tume ya kuwaajiri walimu nchini pamoja wizara husika ya elimu kuita kikao na kujadili suala la mgomo wa walimu, badala ya kuchukua hatua kama hiyo ambayo itaathiri wanafunzi.

Kwa upande wake, msimamizi mkuu wa shule ya akademia ya Joy Educational Centre iliyoko katika mji wa Magena kaunti ya Kisii, Samson Ogega aliishtumu serikali kwa kuwachezea walimu kila mara, na kumtaka rais Uhuru Kenyatta kuheshimu ahadi aliyowapa wakenya wakati akitafuta kiti cha urais kuwa ataheshimu katiba ya Kenya na kuilinda, badala ya kuendelea kulipigia siasa suala la walimu.

Mwalimu huyo wa zamani alisema kuwa kufuatia siasa kama hizo mbaya ndio maana sekta ya elimu inaendelea kudorora, na kuwataka walimu wasikome na kupigania haki yao ya kupata malipo na kuishi maisha kama wenzio katika sekta nyingine za serikali.

Alionya kuwa iwapo serikali itaendelea hivyo, huenda kukawa na ukosefu wa wanataaluma wa masuala ya elimu kwa sababu ya dhuluma ambayo baadhi ya wanafunzi wanashuhudia walimu wao wanapitia, hivyo basi kumtaka rais na naibu wake kunusuru taaluma hii muhimu kwa kuwalipa walimu haki yao.