Naibu chifu wa kata ndogo ya Seregeya huko Turbo amesema kuwa shule za msingi zitajengwa katika kila kijiji.
Akiwahutubia waombolezaji kwenye hafla moja ya matanga katika kijiji cha Chepkoilel siku ya Jumamosi, Diana Owano alisema kuwa shule za msingi zitakazojengwa zitawafaidi sana wakazi wa sehemu hiyo.
Owano aidha amewataka wakazi kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono mradi huo ambao ulianzishwa mwaka wa 2013, ambao umepelekea kujengwa kwa madarasa ya kisasa kwenye shule mpya ya msingi ya Chief Banda.
Vilevile, chifu huyo ameyataka makanisa yote ambayo yatapewa usimamizi wa shule hizo kufanya bidii ya maendeleo na kukuza viwango vya elimu katika eneo hilo.
Mipango ya ujenzi wa shule katika kijiji cha Chepkoilel unaendelea na utafadhiliwa na hazina ya ustawi maeneo bunge nchini, CDF.
"Tumeandikia kamati ya CDF barua na wamesema watatupa pesa za kununua uwanja ili kuhakikisha kuwa shule hiyo inajengwa kwa haraka,” alisema Owano.
Owano alisema kuna mipango maalum ambayo afisi yake imeweka ili kuhakikisha kuwa kila kijiji kwenye kata ya Seregeya kitapata shule ya msingi na ikiwezekana hata ya upili.
"Tunaenda kujenga shule katika kila kijiji ili watoto wetu wapate nafasi nzuri za kusoma na hata kucheza na pia kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye shule chache zilizoko eneo hilo,” alisema Owano.