Mbunge wa Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii Richard Tong’i amefadhili baadhi ya shule za msingi katika eneo bunge lake vitabu vya kusoma.
Hii ni baada ya shule hizo kukiri kuwa hazikuwa na vitabu vya kutosha jambo ambalo lilimlazimu mbunge huyo kuzinunulia shule hizo vitabu hivyo.
Mbunge huyo alizifadhili shule hizo vitabu hivyo siku ya Alhamisi huku akiomba wanafunzi kutia bidii masomoni.
Aidha, mbunge huyo aliwaomba wazazi wote katika eneo bunge lake kuweka motisha kwa kuwasomesha wanao huku akisema uridhi ambao mzazi anaweza mwachia mtoto wake ni masomo.
“Uridhi ambao mzazi anaweza mwachia mtoto ni masomo wala si kingine. Lile ambalo mwastahili mlijue ni kuwa mtoto awe wa tajiri au wa maskini, watakaa meza moja kupitia masomo. Mbona msiwasomeshe watoto wenu?” aliuliza Tongi.
Tong’i alisema kuwa serikali inatoa masomo ya bure na lile ambalo mzazi anahitajika kufanya ni kumnunulia mtoto wake sare ya shule, kalamu na vitabu.
Mbunge huyo alisema kuwa wakati watoto wako nyumbani wasifanyishwe kazi nyingi kwani hawatakuwa na motisha ya kusoma na kusema kuwa wanafunzi wanastahili kupewa muda unaofaa wa kusoma.
“Mtoto kile anahitaji kutoka kwako wewe mzazi ni sare ya shule na kumlisha vizuri ili awe anasikia kile anafundishwa na mwalimu. Serikali ilisema itagharamia pesa za mitihani. Lipi litakuwa ngumu kwenu wazazi? Kila mzazi awajibike kwa kumsomesha mtoto wake,” aliongeza Tong’i.