Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa kaunti ya Mombasa wamehimizwa kuwa makini na kujitenga na siasa za chuki na migawanyiko na badala yake washirikiane na viongozi wao katika ajenda mbali mbali za maendeleo.

Akiwahutubia wakazi wa eneo la Nyali mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Gavana wa kaunti hiyo Hassan Ali Joho alisema kwamba katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa siasa za malumbano ambazo huenda zikaleta ugawanyiko miongoni mwa jamii.

Gavana Joho, alisema kwamba iwapo siasa hizo za chuki zitazidi kuendelezwa katika kaunti hiyo na baaadhi ya wanasiasa na viongozi basi huenda zikakwamisha mchakato wa maendeleo katika kaunti hiyo.

“Tafadhalini wakaazi kuweni makini na mjitenge na baadhi ya wanasiasa na viongozi wapotovu wanaolenga kuwagawanya kisiasa na kikabila kwani hatua hiyo italemaza shughuli za maendeleo katika kaunti yetu”,alisema Joho.

Aidha, alisema kwamba tayari serikali ya kaunti imeandaa mikati mwafaka ya kuendelea maendeleo ya kaunti kwa kubuni ajenda mablimbali za kufanikisha uwekezaji na kukuza uchumi wa mji wa Mombasa na kaunti nzima kwa jumla.

Haya yamejiri huku tofauti kali za kisiasa zikishuhudiwa kati ya gavana Joho na mbunge wa Nyali Hezron Awitti ambaye alikuwa akionekana akiukosoa uongozi wa kaunti hiyo hadharani.

Kulingana na Awiti Serikali ya kaunti ya Mombasa imekuwa ikitumia fedha za umma kiholela huku zaidi ya shilingi milioni 496 kufikia sasa bado hazijulikani ziliko kutokana na kukithiri kwa ufisadi katika kaunti hiyo.