Huku muda wa uongozi kwa kamati ya utekelezaji wa katiba nchini ukitarajiwa kufika ukingoni mwishoni mwa mwaka huu, mwenyekiti wa kamati hiyo Charles Nyachae amesema kuwa hayuko tayari kuteuliwa kuendelea kusimamia kamati hiyo.
Akihutubia hadhara siku ya Alhamisi katika uga wa wa michezo wa Gusii katika hafla ya kutathmini hatua ambazo kamati hiyo imepiga tangu ianzishwe miaka tano iliyopita, Nyachae alisema kuwa hayupo na ari ya kuisimamia kamati hiyo, huku akisema ana shughuli nyingine angependa kufanya ya kuendeleza nchi.
Mwenyekiti huyo alikuwa akijibu wito kutoka kwa viongozi tofauti tofauti, akiwemo gavana wa kaunti ya Kisii na naibu wake ambao waliomba uongozi wa serikali ya Uhuru Kenyatta kumpa awamu nyingine ili afanikishe sera za ugatuzi nchini.
Alisema kuwa yale ambayo amefanya akiwa mwenyekiti wa kamati hiyo ni makubwa, na angependa yeyote ambaye atachukuwa usukani kuhakikisha kuwa sera zote pamoja na sheria zilizotungwa kwenye katiba zinatekelezwa ipasavyo.
Akiongea kwenye hafla hiyo, gavana wa kaunti ya Kisii Bwana James Ongwae alimpa pongezi kiongozi huyo wa CIC, huku akimtaja kuwa mtu mwenye hekima na asiyeogopa anapofanya kazi yake.
Aidha, alimtaka aendelee kuwa na ujasiri kama alioonyesha kwenye miaka mine ambayo amesimamia kamati hiyo.
Ongwae alisema kuwa yeye pamoja na magavana wengine wataendelea kupigania sera na sheria zinazoongoza ugatuzi, na kuwataka viongozi wengine wa kisiasa kuwa na ari na dhamira moja na kupigania ugatuzi nchini.