Spika wa kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki ameagiza wafanyikazi wote ambao waliajiriwa kwa njia ya kutatanisha na kutolipwa kwa miezi 11 iliyopita kutoenda ofisi yoyote ya serikali ya kaunti hiyo kufanya kazi hadi waamrishwe kufanya hivyo.
Akizungumza siku ya Jumatano katika makao ya bunge ya kaunti ya Kisii, Ondieki alisema wafanyikazi hao hawatakubaliwa kuenda ofisi ya serikali ya kaunti hiyo baada ya kusemekana kuwa wafanyikazi ni wengi zaidi walioajiriwa kuliko kiwango kile kilihitajika.
Wakati huo huo, Ondieki alikiri kuwa kati ya wafanyikazi 300 waliopata ajira na kupelekea kutolipwa kwa miezi 11 iliyopita ni wafanyikazi 72 pekee wataajiriwa upya na wengine walipwe na kuenda nyumbani kwani serikali ya kaunti ya Kisii haitawaajiri wote tena.
Ajira ya wafanyikazi hao 300 imekuwa ikizua mdahalo mkubwa kila wakati katika serikali ya kaunti ya Kisii, jambo ambalo lilipelekea spika wa kaunti hiyo kukosolewa vikali na baadhi ya wawakishi wa wadi wa kaunti hiyo na wananchi kwa kutoonyesha uwazi.
Kutolipwa kwa wafanyikazi hao kulipelekea mahakama ya Kisii kuingilia kati baada ya wafanyikazi hao kupeleka malalamishi yao kwa mahakama ambayo ilitoa habari kuwa serikali ilikuwa iajiri watu 72 na wala si 300.