Share news tips with us here at Hivisasa

Huku lawama kuhusiana na wafanyakazi wa kaunti ya Kisii ambao hawajalipwa zikizidi kushika kasi, spika wa kaunti ya Kisii amewataka wawakilishi wa wadi kutoka kaunti hiyo kujiepusha kujadili suala la wafanyakazi waliondamana wiki jana akisema suala hilo liko mbele ya mahakama.

Suala hilo ambalo lilizuka siku ya Jumanne kwenye bunge la kaunti hiyo wakati wa kuchangia mijadala na wawakilishi wadi lilimkera mno spika Kerosi Ondieki, ambapo aliwaonya baadhi ya viongozi ambao walitumia nafasi yao kuongelea suala lililo nje ya mada ya siku.

Kerosi hasa alimtaka kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo, ambaye pia ni mwakilishi wa Bassi Masige Henry Moracha kuepuka kujitanua na suala hilo kwa kujipa umaarufu wa kisiasa, na kuwataka wahusika kuwa na subira kwani jambo hilo litapata suluhu hivi karibuni.

"Tuache kujinufaisha kisiasa kwa masuala yaliyo mbele ya korti, tujaribu kujizuia huku tukitafuta suluhu la tatizo hili," spika huyo alisihi.

Wawakilishi wadi wengi walitishia kuwa hawataingia katika afisi zao mpya ikiwa serikali ya kaunti ya Kisii, hasa spika, atakosa kulishughulikia suala la kulipa wahudumu hao pesa zao za miezi kumi.