Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Ardhi nchini Mohammed Swazuri amesema kwamba shughuli ya kupeana hati miliki kwa shule zote nchini inaendelea.

Kulingana na Swazuri, zaidi ya takriban shule elfu 28 zimetuma maombi kwa tume hiyo ili kupata stakabadhi hiyo muhimu ya shule na akasema kwamba hatua hiyo ni muhimu kwani miaka mingi ardhi za shule zimekuwa zinatambuliwa kuwa ardhi za umma.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Swazuri alisema kwamba mpango wa kutoa hati miliki kwa mashule za umma utapunguza kwa kiasi kikubwa unyakuzi wa ardhi za shule huku akisema kuwa kupatikana kwa stakabadhi hiyo muhimu kutaimarisha shughuli zingine shuleni.

“Mpango wa kutoa hati miliki za ardhi kwa shule za umma nchini kutasaidia kupunguza unyakuzi wa ardhi za shule kwavile ardhi nyingi bado zinatambuliwa kuwa ardhi za umma,” alisema Swazuri.

Aidha, alisema kwamba tume hiyo imesaidia pakubwa katika kuzinusuru baadhi ya ardhi za shule zilizonyakuliwa na baadhi ya mabwanyenye.

Aliwaonya madalali kuwa atakayepatikana akinyakua ardhi ya shule atakabiliwa kisheria.

Swazuri alisema kwamba baadhi ya viongozi nchini waliyo ushawishi serikali wameanza kampeni ya kulishinikiza bunge la kitaifa kupitisha mswada bungeni wa kuivunja tume hiyo na kupata nafasi ya kuwadhuluma wananchi.

“Kuna baadhi ya watu nchini waliyo na ushawishi katika serikali wanaoipiga vita tume ya ardhi ili bunge lipitishe mswada bungeni tume ya ardhi ivunjiliwe mbali ili wapate nafasi ya kuwadhulumu wananchi. Hilo halitawezekana,” alisema Swazuri.

Mwenyekiti huyo aliwaonya baadhi ya wabunge wanaoshinikiza kuvunjiliwa mbali kwa tume hiyo ama kupunguziwa mamlaka akisema kwamba hatua hiyo huenda ikalemaza shughuli za kutatua mzozo ya ardhi nchini.