Baada ya uhaba wa maji kushuhudiwa katika Kaunti ya Mombasa kwa muda wa majuma mawili sasa, kampuni ya usambaji maji katika kaunti hiyo imewahakikishia wakazi kuwa huduma hiyo itarejea hali yake ya kawaidi.
Kulingana na Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Rajab Kombo Rajab, tatizo hilo limetokana na wakazi kujiunganishia mabomba ya maji bila idhini, huku akisema kwamba watakaopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Rajab alisema kwamba wasimamizi wa kampuni hiyo watahakikisha kuwa wakazi wa Mombasa wanapata huduma bora sambamba na maji safi ili kuona kwamba swala hilo linatatuliwa vyema.
“Tatizo la uhaba wa maji mjini Mombasa lilitokana na kukithiri kwa visa vya uunganishaji maji kwa njia ya mkato bila ya idhini, hali ambayo imechangia mabambo ya maji kukumbwa na hitilafu. Hata hivyo, swala hilo limepata suluhu,” alisema Kombo.
Kombo aliwaonya wakazi wanaojifanya kuwa wanakandarasi na kujiunganisha maji kwa njia ya ulaghai kuwa watachukulia hatua kali za kisheria.
Aliwataka wakazi kushirikiana na maafisa wa kampuni hiyo kuwatambua watu hao ili waweze kutiwa nguvuni.
“Tunawaomba wakazi mutupe habari kuhusu watu ambao wanajiunganishia maji kwa njia ya ulaghai ili maafisa wa polisi wawatie nguvuni na kusitisha wizi huo unaoenndelea katika kaunti ya Mombasa,” aliongeza Rajab.
Rajab alisema kwamba kampuni hiyo imeimarisha huduma zake na kuahidi wakazi wa kaunti hiyo kutokumbwa na changamoto za uhaba wa maji kwani mitambo imerekebishwa na huduma za usambazaji maji zimeimarishwa.