Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko ameshinikizwa kuwakabili vikali viongozi na wanasiasa wanaotoa matamshi yanayolenga kuwagawanya wakenya.
Kulingana na Kiongozi wa chama cha Tip Tip Kalembe Ndile, baadhi ya viongozi humu nchini wanatoa matamshi ya chuki na wanastahili kukabiliwa vikali ili kuzuia mifarakano katika taifa hili.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kalembe alisema kwamba matamshi yaliyotolewa na Seneta wa Machakos Johnstone Muthama, Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria na mwanasheria na mchanganuzi wa maswala ya kisiasa Mutahi Ngunyi yanafaa kuchunguzwa kwa kina, na viongozi hao kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kwani matamshi yao huenda yakasababisha migogoro.
“Tungemuomba Tobiko aagize uchunguzi wa kina kwa viongozi hao dhidi ya matamshi yao waliyotoa katika mikutano ya hadhra na ikiwezekana wafanyiwie uchunguzi wa kiakili, huenda wakawa na shida flani kwani matamshi wanayotoa yanaweza kuwagawanya wakenya,” alisema Kalembe.
Wakati huo huo, amewataka viongozi wa mrengo wa Cord kukoma kukashifu serikali hususan kuhusiana na swala la mishahara ya walimu, na badala yake wajadili mambo yanayoweza kulijenga taifa.
“Viongozi wa mrengo wa Cord wajitokeze na watuambie hii pesa waliitisha kuchangisha imefika ngapi na wamepanga vipi kuwasaidia walimu sio tu kutwambia tuchange na baadhi ya viongozi tunawajua mambo yao kuwa wanalenga kutumia hiyo pesa kwa kampeni," aliongeza Kalembe.
Tayari, mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko ametaka kufunguliwa mashtaka mara moja kwa Ngunyi, baada ya juhudi zake za kuzuia kutiwa nguvuni kugonga mwamba.