Share news tips with us here at Hivisasa

Uchukuzi kwa kutumia magari aina ya Tuktuk umeendelea kuwa maarufu Kisumu huku abiria wengi na wafanyibiashara wakipendelea kuyatumia kutokana na starehe zake za kipekee. 

Kulingana na wachuuzi katika jiji hili, tuktuk ni rahisi kuabiria na kubebea mizigo, hali ambayo wanasema kuwa inawarahisishia biashara na usafiri. 

Wanasema kuwa magari hayo ni rahisi kupenya katika maeneo ambayo sio mapana na husonga kwa wepesi wakati wa msongamano. 

Mary Akumu ni mfanyibiashara wa miaka mingi jijini hapo ambaye anasema kuwa huduma za tuktuk kwake ni za heri. Anasema kuwa magari hayo yanarahisisha kazi yake kwa kufika kila kona anakotaka na kwa wakati, huku yakiwa na uwezo wa kubeba mizigo. 

''Mimi wakati mwingi natumia tuktuk kwa kusafirisha mizigo nikienda sokoni. Ni rahisi kuabiria na inatusaidia kufika kila kona na kwa wakati,'' alisema Akumu Jumamosi jijini Kisumu. 

Tofauti na pikipiki, tuktuk ina sehemu ya nyuma ya kubebea mizigo (buti), ambayo inawafanya wafanyibiashara wengi kupendelea uchukuzi wake. 

Mbali na wafanyibiashara kupendelea huduma za magari hayo, abiria wengi hupenda kuyatumia wakati wanapohitaji kufika haraka huku wakitumia hela kidogo kwa nauli ya chini kushinda pikipiki.