Mkuu wa Idara ya utalii na utamaduni katika Kaunti ya Mombasa Joab Tumbo amesema kwamba wizara yake itashirikiana kwa ukaribu mno na wadau katika sekta ya utalii ili kuona kwamba sekta hiyo inaimarika kikamilifu.
Akiongea na wanahabari afisi mwake siku ya Jumatatu mjini Mombasa, Tumbo alisema kwamba kupitia kwa ushirikiano, huenda sekta hiyo ikafanikiwa kurudi katika hali yake ya awali, licha ya kuwepo kwa changamoto za kiusalama ambazo ziliweza kuididimiza sekta hiyo kwa muda.
Tumbo alisema sekta hiyo iliathirika pakubwa katika kipindi ambacho mataifa ya ulaya yaliweka marufuku kwa raia wao kutozuru humu nchini lakini kuondolewa kwa marufuku kwa baadhi ya mataifa kumesaidia sekta hiyo kukua kwa kasi.
“Sekta ya utalii kwa sasa imeanza kurejea hali yake ya kawaida baada ya kukumbwa na changamoto za kiusalama zilizosababisha baadhi ya mataifa ya ulaya kuwazuia raia wao kuzuru humu nchii na kudidmiza sekta hiyo. Lakini kwa sasa, tunalotumaini la kuimarika kwa utalii kwani tunapanga kushirikiana na wadau katika sekta hiyo,” alisema Tumbo.
Tumbo aliongeza kuwa tamaduni za kipwani zinazoendelezwa na wakazi mashinani na maandari ya kuvutia mjini Mombasa zitachangia pakubwa katika kuwavutia watalii kuzuru eneo la Pwani hali itakayopelekea sekta hiyo kuimarika
“Tayari wakazi wa Pwani wanaendeleza juhudi za kukuza utamaduni wao kama njia moja wapo ya kuwavutia watalii kuutambua utamaduni wetu na kupata pato ambalo litawawezesha wakazi kujikimu kimaisha,” aliongezea Tumbo.
Wakati huo huo, Tumbo alitoa shinikizo kwa wakazi katika kaunti hiyo kuukuza utalii wa kipwani katika ukanda wa Pwani ili kuwavutia watalii wengi zaidi.