Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Tume ya kitaifa ya Ardhi imetakiwa kutekeleza majukumu yake jinsi ipasavyo ili kuhakikisha kuwa mizozo ya ardhi kwa wakazi wa Kaunti ya Mombasa inatatuliwa.

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mipangilio ya mji katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya, alisema kuwa tume hiyo haijawahi kushinda kesi hata moja ya kutatua mzozo wa ardhi inayowahusu wakazi mashinani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Thoya alidai kwamba baadhi ya maafisa wa tume hiyo kwa ushirikiano na maafisa wa utawala wamekuwa wakishirikiana na mabwanyenye katika kuwafurusha wakazi katika ardhi zao wanazomiliki baada ya kupewa hongo.

“Sijawahi ona siku hata moja Tume ya kitaifa ya Ardhi ikishinda kesi za mzozo wa ardhi katika Kaunti ya Mombasa. Tume hiyo huwaambia Wakenya wawe na subira lakini wakazi huwa hawaoni matunda ya subira hiyo,” alisema Thoya.

Thoya aliahidi kushirikiana na wakazi katika kaunti hiyo kuishinikiza serikali kuingilia kati swala la unyakuzi wa ardhi ili kuona kwamba wakazi wanaishi katika ardhi zao bila hofu ya kufurushwa.

“Tutaungana pamoja na kuishinikiza serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa kuingilia kati swala la mzozo wa ardhi na ili wakazi waweze kuishi bila hofu. Hili swala la kuzozana kila siku halitasaidia wakazi hata kidogo,” aliongezea Thoya.

Aidha, aliwataka wakazi kutoyahama makazi yao wala kushauriana na viongozi wenye malengo potovu kwa kuwahadaa na fedha kidogo ili kuyahama makazi yao kwani itawasababishia shida katika siku za usoni.

Swala la mzozo ya ardhi katika Kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani limekuwa changamoto kubwa hata baada ya serikali kuahidi kuwapa wakazi hati za kumiliki ardhi.