Wahudumu wa bodaboda za baiskeli mjini Kisumu wamenuia kuboresha huduma zao kwa madhumuni ya kufanikisha uchukuzi mjini.
Uchukuzi wa bodaboda za baiskeli katika pembe nyingi nchini ulidumu kwa miaka mingi na ukawa maarufu kwa wasafiri kabla ya kuweko kwa huduma za uchukuzi za kisasa za pikipiki.
Wahudumu hao kupitia kwa chama chao cha waendeshaji wa baisikeli hizo za uchukuzi mjini Kisumu, wamesema kuwa mengi yanatarajiwa kufanywa kuboresha uchukuzi huo ambao umeonekana kudidimia.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi mjini Kisumu, mwenyekiti Moses Nyawara alisema kuwa chama chao kimenuia kufadhili kila mwanachama kwa kununua baiskeli mpya kwa kila mmoja pamoja na vifaa za mapambo kwa starehe za wateja wao.
''Wakati umewadia ambapo kila kitu kinastahili kubadilika kulingana na mazingira. Tunaendelea kutafuta msaada kutoka kwa wadhamini ili kuboresha huduma zetu,'' alisema Nyawara.
Nyawara alidokeza kuwa kulingana na ustarabu wa wateja, ni lazima baiskeli za bodaboda ziwekewe mapambo na viti vyenye godoro na taa kwa burudani na usalama kamili kwa wateja wao.
Ingawa uchukuzi wa pikipiki ni maarufu sana na tegemeo la wasafiri wengi jijini Kisumu, wenye baiskeli nao hawakosi kupata wateja kutokana na nafuu ya nauli inayotozwa na bodaboda hizo.