Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa afya katika kaunti ya Machakos Naomi Mutie amesema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichosababisha vifo vya watoto sita katika hospitali ya Kangundo Level Four.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika mazishi ya ndugu ya waziri wa mambo ya ugatuzi katika kaunti ya Machakos Lukas kioko katika eneo la Katulu, kaunti ndogo ya Matungulu kaunti ya Machakos, Mutie alisema kuwa ni jambo la kushangaza kwa mama kumpoteza mtoto siku moja baada ya kujifungua kwa njia zisizoeleweka. 

"Furaha ya mzazi ni kujifungua vizuri na kumpakata mwanawe mikononi mwake, kumlea kuona kila hatua anayopiga, lakini ni jambo la kutamausha sana kumpoteza mtoto saa chache baada ya kumpakata," alisema Mutie. 

Waziri huyo aliahidi umati uliofika kuwa uchunguzi wa kina utaendelezwa haraka ipasavyo na watakaopatikana na hatia kufunguliwa mashtaka hatua, iliyoungwa mkono na Mbunge wa Matungulu Stephen Mule. 

"Uchunguzi wa kina utaanzishwa kubaini nini kilisababisha vifo hivi, na yeyote atakayepatikana na makosa kufikishwa mahakamani ili haki itendeke," aliongezea Mutie. 

Haya yanajiri siku mbili baada ya watoto sita kupoteza maisha yao katika njia za kutatanisha katika hospitali ya Kangundo. 

Vilevile, waziri huyo aliwapa pole wazazi waliofiwa na watoto wao katika kisa hicho.