Share news tips with us here at Hivisasa

Ufisadi katika Idara ya usajili wa watu nchini umetajwa kuchangia pakubwa ukosefu wa usalama na ongezeko la vijana kujiunga na vikundi ya itikadi kali.

Akizungumza na wanahabari katika afisi za tume ya kitaifa la utawala wa haki nchini siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa tume hiyo Otiende Amollo alisema kuwa idara za serikali nchini hususan idara ya usajili wa watu imechangia kuwepo kwa ukosefu wa usalama humu nchini.

Amollo amesema utafiti uliyofanywa na tume hiyo katika kipindi cha mwaka moja umebaini kuwa ufisadi katika idara za serikali ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama pamoja na kuwepo kwa vijana wadogo kujiunga na makundi ya itikadi kali.

“Ripoti tuliyonayo leo imeonyesha wazi utafiti uliyofanywa na maafisa wa tume hii walipozuru mashinani na kuongea na wakazi umebaini kuwa maeneo ya Lamu, Samburu na mjini Mombasa ndio yaliyoathirika zaidi na kashfa za ufisidi,” alisema Amollo.

Amollo ameitaka tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC kuingilia kati swala hilo na kuhakisha kuwa wanazuru hadi mashinani na kuwachunguza maafisa wanaoshiriki ufisadi ili kuwafungulia mashtaka.

Aidha, amesema kuwa utafiti huo umebaini kuwa wakazi hupitia changamoto nyingi kabla ya kupata stakabadhi muhimu za umma ikiwemo vitambulisho, vyeti vya usafiri na vile vya kuzaliwa hali ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.

“Maafisa wa idara za kiserikali haswa idara ya usajili wa watu ndio wamechangia kwa kiwango kikubwa ukosefu wa usalama kwa kuitisha hongo kabla ya kuwasajili watu kupata vitambulisho,” alisema Amollo.

Tume hiyo imeorodhesha kupokea kesi 1, 730 ambazo wanatarajia kukamilisha uchunguzi wao kabla ya kuziwasilisha mahakamani.