Share news tips with us here at Hivisasa

Biashara ya pombe haramu pamoja na uuzaji wa mihadarati katika eneo la Ahero na kituo cha kibiashara cha Bahati ni tishio kubwa la kiusalama.

Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa wilaya Macharia Njinu, aliyekuwa akizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa, ambapo alisema kwamba operesheni kali itafanywa maeneo hayo ili kusaka wauzaji wote wa pombe na mihadarati.

Bwana Njinu hata hivyo alitoa wito kwa viongozi wa nyumba kumi kushirikiana kumaliza uuzaji wa pombe kwenye handaki moja la muuzaji sugu kwa jina Nyambura, ambaye amekuwa akikwepa mtego wa polisi.

“Huyu mama amekuwa akikwepa polisi kila mara tunapomwendea, ingekuwa ni bora wale ambao wanajua saa ambayo anauza, wafahamishe viongozi wa nyumba kumi ili washirikiane na polisi kumkamata,” alisema afisa huyo wa serikali.

Kulingana na uchunguzi wa mwandishi huyu, wengi wa wanaouza mihadarati hiyo huisafirisha kwa pikipiki, na hivyo inakuwa vigumu kwa polisi kuwatambua.

Aidha, pombe nyingi inayouzwa wilayani Nakuru kaskazini hutoka maeneo ya Kwa-Rhonda, Section 58, na Kaptembwa, maeneo yaliyo Nakuru mjini.

Bwana Njinu pia amechangamoto wananchi kutoa habari pia kwa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya nchini Nacada, katika kumaliza tatizo hilo.

“Baadhi ya vijana ambao hufanya kazi na malori ya mawe hawana hata mahala pa kulala, wao hulala kwenye mashimo hayo ambalo pia ni tatizo kwa usalama haswa wa akina mama na wasichana wa shule. Kama wanaogopa kuandikisha taarifa kwa polisi, basi waipe Nacada vidokeo kuhusu washukiwa wa dawa na pombe, ili wakamatwe,” aliongeza  Macharia.