Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kisii Mary Sally Otara amewaomba vijana na akina mama kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura.
Mwakilishi wa wanawake Otara alisema kujiandikisha ndio njia pekee ya kupata fursa ya kuwachagua viongozi wafaao ifikapo mwaka 2017 na hata kuwa na thibitisho kuwa Mkenya.
Akizungumza mnamo siku ya Jumapili katika mji wa Kisii alipokuwa akitoa habari njema ya kupambana na funza ambao wameathiri baadhi ya familia katika sehemu mbali mbali za Kaunti ya Kisii, Otara alisema kura ndio silaha muhimu ya kuhakikisha viongozi wazuri wenye ndoto ya kufanya maendeleo wamechaguliwa.
Wakati uo huo, Mwakilishi huyo aliongeza kuwa kujiandikisha kwa wingi huwa kunasaidia vijana kukabidhiwa pesa za mikopo, haswa Uwezo Fund na zinginezo ili kufanyia biashara zao kuinua uchumi na kujiimarisha kimaisha huku akikariri kuwa pesa nyingi zitatoka kwa serikali kuu uenda katika Kaunti mbali mbali.
“Nawaomba kila mtu haswa vijana kupata vitambulisho kwa wingi ili tuweze kuwachagua viongozi walio na maono ya kufanya maendeleo,” alisema Otara, Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kisii.
Aidha, Otara aliwaomba vijana walio na vitambulisho kuendelea kueneza habari ya kupasha wengine katika sehemu mbali mbali umuhimu wa kuchagua viongozi wa kutekeleza maendeleo kwa wananchi.