Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Vijana kutoka wadi ya Kemera, kaunti ya Nyamira, wameombwa kukumbatia ufugaji wa sungura kama njia mojawapo ya kujiajiri. 

Kulingana na mkulima mmoja wa eneo hilo, Douglas Rayori, ambaye amekuwa akifuga sungura hao kwa miaka nne sasa, ufugaji wa sungura umemletea faida kubwa baada yake kutafuta kazi kwa miaka miwili bila mafanikio, huku akiongezea kuwa ufugaji huo umeimarisha mapato yake kwa kuwa sungura hao wana soko humu nchini na katika mataifa ya kigeni.

"Ufugaji wa sungura umeniletea faida kubwa kwa kuwa sungura hao wanaagizwa kwa kiwango cha juu humu nchini na hata pia kwenye mataifa ya kigeni," alisema Rayori. 

Mkulima huyo aliongezea kwa kusema kuwa alipoanzisha biashara ya ufugaji huo wa sungura angeuza sungura mmoja kwa shillingi mia tatu, lakini kwa sasa sungura mwenye kimo kidogo huuzwa kwa shillingi mia saba, huku yule mkubwa akiuzwa kwa takriban shillingi elfu tatu.

"Vijana wengi wanaendelea kutafuta ajira bila mafanikio ilhali wanaweza fuga sungura ili kuimarisha mapato yao, kwa sababu nilipoanza biashara hii miaka mitatu iliyopita, nilikuwa nauza sungura mmoja kwa shillingi mi tatu, lakini kwa sasa mapato hayo yameimarika hata zaidi," aliongeza Rayori.

Mkulima huyo aidha amethibitisha kuuza zaidi ya sungura 15 kwa mwezi, hali anayoitegemea kukimu familia yake. 

"Kwa mwezi naeza uza zaidi ya sungura 15 hali inayonisaidia kukimu familia yangu," alisema Rayori.