Kiongozi wa vijana katika wadi ya Marani eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini, amewaomba vijana kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura ili kuwachagua viongozi watakao leta maendeleo na kubadilisha uongozi ifikapo mwaka wa 2017.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika wadi hiyo ya Marani alipokuwa anatembelea miradi ya maendeleo inayofanywa na vijana katika vikundi mbalimbali katika wadi hiyo, Daniel Obiri alidai kuwa wengi wa viongozi walio mamlakani hawakumbuki vijana kwa kuwahusisha kimaendeleo katika maeneo wanayoyawakilisha.
“Naomba kila kijana ambaye hana kitambulisho apate kitambulisho chake tusiache yeyote nyuma tunapoenda kubadilisha uongozi,”alisema Obiri.
Aliongezea, “Serikali imejitolea kuwapa vijana vitambulisho bila malipo na hivo basi tusikose kuchukuwa vitambulisho.”
Obiri alisema kuwa vijana wengi huachwa nje wakati wa kupiga kura kwa sababu hawana vitambulisho, huku akisema kuwa kukosa kushiriki kwenye uchaguzi wa viongozi nchini ni kukosa haki ya kikatiba nchini na kukiuka sheria.
“Naomba machifu na manaibu wao kuwatangazia wananchi kuhusu baraza zao na kuhimiza vijana walio na umri wa miaka 18 kuchukuwa vitambulisho kwani wengi huachwa nje wakati kama huu kwa sababu za kutokufahamishwa yanayojiri nchini kenya,” aliosema Obiri.