Vijana kutoka Kaunti ya Mombasa wameonywa dhidi ya kujihusisha na uhalifu na ulaghai ambao huenda ukawaweka matatani na hata kupoteza maisha huku wakazi wakitakiwa kuwa macho.
Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Kamanda wa Polisi katika kanda ya Pwani, Francis Wanjohi, alisema kuwa vijana wengi kutoka eneo hilo wamependa kupata mali kwa njia za mkato na kukosa kufanya shughuli halali za kuwapa riziki.
Kamanda huyo aliwataka wazazi kuwa makini na kuwashauri watoto wao njia muhimu na kuhakikisha kuwa wanakuwa na habari kuhusu vikundi na aina ya rafiki ambao watoto wao hujihusisha na wao ili kuwaepusha mapema kujiingiza katika magenge hatari.
Pia, ametoa onyo kali kwa wakazi hasa vijana ambao huwaangaisha wakazi wa kaunti hiyo hasa maeneo ya Old Town, Majengo na mitaa mingine katika jiji hilo lenye sifa ya utalii.
Amesema haya siku chache baada ya wakazi kutoka mitaa mbali mbali kutoka kaunti ya Mombasa kutoa lalama kuwa kuna vijana ambao wanazunguka na kuwalaghai wakazi pesa zao, na wengine kusemekana kuzunguka katika nyumba za makazi kwa kutumia vitambulisho bandia vya polisi ambapo hujifanya maafisa wa polisi na kuwaibia wakazi vitu vya nyumba na kuwapiga wanaokaidi kufuata maagizo yao.