Vijana katika Kaunti ya Nyamira wameombwa kufanya maamuzi ya busara hasa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Kulingana na katibu mratibu wa Chama cha KPAWU Bw Henry Omasire, aliyekuwa akiwahutubia waumini wa kanisa la kiadventista kwenye hafla yakuchangasha pesa za ujenzi wa kanisa kule Omokonge siku ya Jumapili, vijana wengi hutumiwa vibaya na wanasiasa wakati wa uchaguzi, hali inayosababisha viongozi wasio stahili kuchaguliwa kuongoza kwenye nyadhifa za kiasasa.
"Vijana wengi hutumiwa na wanasiasa hasa kwenye msimu wa uchaguzi kwa kununuliwa vileo. Hali hiyo husababisha vijana kufanya maamuzi yasiyo ya busara kwenye uchaguzi, na huishia kuwateuwa viongozi wasio stahili kuwa mamlakani,” alisema Omasire.
Katibu huyo wa Chama cha KPAWU kilichoko chini ya mwavuli wa COTU alisema kuwa sharti vijana wajiepushe na vishawishi vinavyo weza kuwaharibia maisha yao ya siku za usoni.
"Iwapo vijana watawachagua viongozi wasio stahili, huenda maisha yao yakaharibikia,” alisema Omasire.
Akizungumzia swala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, Omasire alisema kuwa yafaa vijana kubuni mbinu zakupata ajira badala yakungoja kuajiriwa.