Mkuu wa idara ya mipangilio ya miji na ardhi katika Kaunti ya Kisii Moses Onderi amewasihi vijana wa kuosha magari kwenye mji wa Kisii na viungani vyake wameombwa kuhifadhi usafi kwa kukoma kuchafua Mto Nyakumisaro.
Akitoa wasia huo Ijumaa katika ofisi yake, Onderi alistaajibikia hali na hulka miongoni mwa vijana hao wa magari kumwaga mafuta ya gari na taka kwenye mto huo, kitendo ambacho alikisema kinaathiri wengi hasa wanaoishi karibu na mto huo na kuyatumia maji ya mto huo kwa shughuli za kinyumbani.
Japokuwa Onderi alikiri kuwa vijana hao hujitafutia hela kwa kazi ya kuyaosha magari, aliwaomba baadhi yao hususan wale wanahudumu karibu na daraja la barabara ya Prisons-Ram kutoa vikingi ndani ya mto huo ambavyo huziba bomba la kupitisha maji na kusababisha maji kugharika na kuenea juu ya barabara na kuwatatiza watu na magari pamoja na wahudumu wa bodaboda ambao hutumia daraja hilo hasa nyakati za mvua.
Aidha, Onderi aliwashukuru wakazi wa kaunti hiyo ambao wamekuwa kwenye mstari wa mbele kuona kuwa miji yote ya kaunti hiyo ipo katika hali ya kuridhisha kwa usafi.
Kwenye siku za hivi karibuni waziri Onderi pamoja na gavana wa Kisii James Ongwae na Mbunge wa Kitutu Chache ya Kati Richard Onyonka waliwaongoza wakazi pamoja na vijana wa Huduma Kwa Taifa (NYS) kuweka usafi kwenye soko la Daraja Mbili iliyoko mjini Kisii.
Wito huu unakuja tu wakati ambapo serikali ya Kaunti ya Kisii inatia juhudi za kuhakikisha mji wa Kisii na mazingira kwa jumla ni masafi.