Vijana katika eneo la Zambezi, kaunti ndogo ya Kikuyu wamelalamikia kusumbuliwa na maafisa wa polisi wanapoendeleza biashara zao kwa kushukiwa kuwa wezi.
Akizungumza siku ya Ijumaa, mwakilishi wa vijana katika eneo la Zambezi, Bwana Erickson Kariuki, alisema kwamba vijana wamelalamikia kutokuwepo kwa amani wanapoendeleza biashara zao kwa madai ya kusumbuliwa na polisi.
Alisema kuwa jambo hilo limewasababisha baadhi ya vijana hao kufunga biashara zao kwa kuhofia kukamatwa.
Kariuki alisema kwamba vijana wengi katika eneo hilo wamekuwa wakijikimu kimaisha kwa kufanya biashara zao na sio vyema kwao kulazimika kufunga bishara hizo wanapoanza kushukiwa na maafisa wa usalama.
Hata hivyo, alieleza kwamba kuna vijana ambao wanajihusisha na shughuli zinazokiuka sheria bali sio wale wanaofanya biashara zao.
Alisema polisi wanapoendeleze oparesheni yao ya kudumisha usalama, wasiwakamate vijana kiholela bila sababu kamili.
"Mimi kama mwakilishi wa vijana katika eneo hili nawaomba maafisa wa usalama wawe makini wanapofanya oparesheni yao na kuwakamata wale wanaotekeleza uovu. Sio vijana wote katika eneo hili wanaokiuka sheria," alisema Kariuki.
Alielezea kwamba vijana hao wako tayari kushirikiana na polisi kwa kuwapa habari kuhusu wanaotekeleza uovu kwa kuwa wao pia wanaathirika na tabia ya vijana wahalifu.
“Vijana hawa wanaofanya biashara ni wale ambao wameokolewa kutoka dawa za kulevya na wamepokea mafunzo ya kibiashara ili kubadilisha maisha yao na pia kujikimu,” alisema Kariuki.