Viongozi kutoka Kaunti ya Garissa wameitaka serikali kuu kukifungua Chuo Kikuu cha Garissa kilicho shambuliwa na magaidi wa kundi la Al Shabaab miezi minne iliyopita.
Wakiongozwa na Gavana wa Garissa Nathif Jama siku ya Jumatatu katika hafla ya kuadhimisha miezi minne baada ya shambulizi hilo katika chuo hicho, walisema kuwa hatua ya serikali kuendelea kukifunga chuo hicho inaonyesha imeshindwa na vita dhidi ya ugaidi, jambo ambalo si sahihi.
Jama aliongeza kuwa serikali lazima itatue kiini cha tatizo la ugaidi nchini ambacho ni ufisadi ambao umelemaza juhudi za kuimarisha usalama katika eneo hilo.
"Serikali ni sharti itafute suluhu kwa changamoto ya utovu wa usalama ambao ni ufisadi," alisema Jama.
Viongozi hao waliiomba serikali kukifungua chuo hicho huku wakisema kuwa kuendelea kukifunga kunalemaza juhudi za masomo katika eneo hilo.
Naibu Gavana Garissa Abdullahi Hussein na mbunge wa Lagdera Mohamed Shidiye pia walikuwepo.