Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi mbalimbali kutoka eneo la Kisii wakiongozwa na aliyekuwa mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii, Robert Monda, wamemuomba Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati swala la mishahara ya walimu ili walimu kupata haki na kurudi madarasani.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wanafunzi wanaendelea kuteseka hasa wale ambao wanaenda kufanya mtihani wa kitaifa mwaka huu.

Monda ameomba Rais kenyatta kuagiza tume ya kuajiri walimu nchini TSC, kuwalipa walimu kulingana na agizo la mahakama lililotolewa hapo kuwa walimu walipwe kati ya asilimia 50 hadi 60 ya mishahara.

Akizungumza siku ya Jumapili katika hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa nyumba ya kasisi wa Amasago eneo bunge la Nyaribari Chache, Robert Monda na viongozi wengine waliomba Rais Kenyatta kuongeza walimu mishahara yao ili kurudi darasani jinsi ilivyoagizwa na mahakama kuu nchini.

“Tunaomba Rais Kenyatta kuongeza walimu mishahara kwani wanafunzi wamesumbuka sana na hata wazazi wamehofia kuwa huenda wanafunzi wasipite mitihani,” alisema Monda.

Kufikia sasa, ishara zimeonekanaa kuwa tume ya kuwajiri walimu nchini TSC na wizara ya elimu haijakubali agizo la mahakama hadi sasa.

Ombi hilo liliungwa mkono na viongozi kama mwenyekiti wa Kenyatta International Convention Centre James Omingo Magara, Henry Obwocha, Chris Bichage, Samel Nyangeso na wengine wengi.

Zaidi ya Sh800,000 zilichangishwa katika sherehe hiyo ambazo zitasaidia ujenzi wa nyumba ya kasisi kukamilika.