Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa kiislamu wa baraza kuu la kiisilamu la 'Sufi Supreme Council of Kenya’ limejitolea kuzuru kaunti zote za pwani ili kuwanusuru vijana waliyojitosa katika utumizi wa mihadarati.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kongamano la viongozi wa dini, Katibu wa baraza hilo Omar Mohammed Omar alisema kwamba ni lazima kwa viongozi wa kidini kuungana na serikali katika kupiga vita utumizi wa dawa za kelevya katika eneo zima la Pwani.

Omar aliwashinikiza maafisa wa usalama kujizatiti zaidi katika kuwakabili walanguzi wakuu wa mihadarati eneo la Pwani na haswa katika kaunti ya Mombasa, inayotajwa kuathirika zaidi na dawa za kulevya kwa vijana wadogo, swala ambalo linahitaji kusitishwa.

“Tumeungana hapa kujadiliana jinsi ya kusitisha kukithiri kwa mihadarati katika kaunti zote za pwani na hususan kaunti ya Mombasa kwani ndio kaunti ambayo iko na idadi kubwa ya vijana waliyojitosa katika janga hilo,” alisem Omar.

Naye Mwenyekiti wa Baraza hilo Abdulkadir Said Al ahdaly alisema kwamba tatizo hilo limechangiwa pakubwa na vijana kukosa malezi bora pamoja na msingi wa dini katika jamii, huku akiahidi kuzuru mashinani na kujadiliana na vijana ili kuwanasua katika jinamizi hilo.

“Tatizo la vijana kutumia mihadarati limechangiwa na idadi kubwa ya vijana kukosa elimu ya dini kuanzia wangali wadogo pamoja na malezi bora kutoka kwa wazazi wao, hatua ambayo kama haitashughulikiwa basi vijana wengi watazidi kuangamia. Ndiposa sisi kama viongozi wa dini tumekubaliana kuzuru mashinani na kuwaelimisha vijana jinsi ya kujiepusha na mihadarati,” alisema Abdulkadir.

Al ahdaly ameiomba serikali itilie manani swala hilo na kushughulika katika kuwatengea ajira vijana wasiokuwa na kazi ili wajishughulishe na miradi mbalimbali itakayowawezesha kujikimu kimaisha na kuzisaidia jamii zao.