Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imeweka mikakati ya kuanzisha vituo vya kurekebisha tabia kwenye gereza la Shimo la Tewa pamoja na magereza mengine ambamo waraibu hao wa dawa za kulevya wamezuiliwa.

Akithibitisha hayo siku ya Ijumaa wakati alipokuwa anawahutubia wanahabari mjini Mombasa, kwenye hafla ya kuzindua utaratibu wa kuwafaa waathiriwa kwenye hospitali ya Coast General, mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa, Binti Omar, alisema kuwa kuna haja ya kuwafaa waathiriwa kwa kujenga vituo maalum kuwapa nasaha jinsi ya kujikwamua kutoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Waziri huyo alisema kuwa shughuli hiyo itafanikishwa na kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na mamlaka ya kupigana na mihadarati nchini ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na watu ambao hawatumii dawa za kulevya na hivyo basi kupandisha uchumi wa nchi kwa jumla.

Aidha, alipongeza juhudi za mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya serikali pamoja na wakazi kwa kutoa ripoti muhimu kwenye idara ya polisi ili kuwachukulia hatua walanguzi ambao alisema wamechangia pakubwa kuzamisha maisha ya wakazi wa Mombasa.

“Ni jukumu la kila mkazi pamoja na Jamii ya pwani kushirikiana ili kuhakikisha kuwa janga la mihadarati litakomezwa kabisa katika kaunti zote za Pwani ambazo zimeathirika,” alisema Omar.

Alitoa wito kwa wazazi ambao wana vijana au jamaa ambao wameathirika kuhakikisha kuwa wanawaandikisha kwenye vituo vya kutoa nasaha.