Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wachonga vinyago katika eneo la Tabaka, eneo bunge la Mugirango Kusini, Kaunti ya Kisii, wameomba serikali ya kaunti hiyo kuwatafutia soko la vinyago hivyo.

Kulingana na wachongaji hao wa vinyago hawajafaidika kutokana na kazi hiyo wanayoifanya kufuatia usimamizi mbaya na kutosaidiwa na serikali vyovyote.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili katika eneo la Tabaka, mwenyekiti wa wachongaji hao Daniel Seme alisema kuwa hawajawai pata msaada wowote kutoka kwa serikali, jambo lililowafanya kusalia kuwa maskini.

Aidha, walisema kupitia uchongaji huo, wameletea serikali ya kaunti ya Kisii sifa kubwa na nzuri, na kufanya kaunti hiyo kujulikana kimataifa, lakini hawapewi msaada wowote.

Walisema kuwa wamejitokeza kuomba usaidizi wa kutafutiwa soko ili wajiendeleze kupitia uchongaji huo.

“Naomba serikali ya Kaunti ya Kisii kutukumbuka na kuweka mikakati maalumu ya kuinua sekta hii yetu ya uchongaji vinyago, kwa kututafutia soko maana wengi wetu tulianza hii kazi mwaka wa 1980 ili tulishe familia, lakini tunaendelea kusalia kuwa katika hali ya umaskini,” alisema Seme.

“Naomba tutafutiwe soko ili nasi tupate msaada, tufaidike na turidhike kwa ile kazi tunayoifanya hapa,” alisema Victor Kerama, mchonga vinyago.