Share news tips with us here at Hivisasa

Wachuuzi wa vyakula katika mji wa Kisii na vyunga vyake wamelalamikia kunyanyaswa na askari wa kaunti hiyo kwa ushirikiano na maafisa wengine wa afya ambao wamekuwa wakiwatia mbaroni.

Wauzaji hao, wakiongozwa na Zetric Bosire, ambaye anasimamia makundi ya wauza vyakula na bidhaa rejareja, walishtumu kisa cha kupigwa na kuumizwa vibaya kwa kijana mmoja wa kuuza mayai ya kuchemshwa katika barabara kuu ya kuelekea soko kuu la Daraja Mbili siku ya Jumanne.

Bosire alitaja kisa hicho kilichoshuhudiwa kama sikitiko sana, na jambo ambalo litaadhiri hali ya biashara katika eneo hilo, huku akisema wengi wa vijana na kina mama wana hofu kubwa.

Msimamizi huyo aliishtumu serikali ya kaunti ya Kisii kwa kukosa kuweka mikakati mahususi ya kuwasiliana na wafanyabiashara hao, akitoa mfano wa kisa hicho na msako huo alioutaja kuwa wa papara.

Kwa upande wake, kijana huyo ambaye alipigwa na maafisa hao alisema kuwa hakuna siku amekosa kulipa ushuru kwenye maafisa wa kaunti, na hawakuwa na habari kuhusu msako huo wa maafisaa wa kaunti.

Aidha, kulingana na mmoja wa vijana ambaye pia huuza mahindi yaliyochemshwa katika eneo la Tuskys, Geseke Mosiori, baadhi ya watu wamekuwa wakijifanya kuwa wahudumu wa afya na wamekuwa wakiwataka kuwapa pesa ndipo wawaruhusu kuendelea na biashara yao.

kitendo hicho kilizua hamaki miongoni mwa vijana wa kuendesha bodaboda pamoja na wafanyabiashara wa bidhaa rejareja katika mji wa Kisii, na kutishia kuandamana ili haki itendeke kwa wenzao.

Hata hivyo, juhudi za mwandishi huyu kutaka kusema na mmoja wa afisa waliosimamia shughuli hiyo hazikufua dafu, kwani alisema hawana idhini na uwezo wa kuongea na vyombo vya habari.