Afisa wa afya katika eneo la Bomu amewataka wahudumu wa kuuza vyakula katika eneo hilo kuzingatia usafi wapouza chukula chao ili kujiepusha na mkurupuko wa maradhi yanohusiana na uchafu.
Akiongea na mwandishi huyu katika mji wa Likoni katika shughuli ya kukagua vibanda vya kuuza vyakula kama vile samaki, matunda na mboga, viazi vya karai na aina nyingine za vyakula siku ya Jumatatu, Joel Akech alisema kuwa afya ya wakazi imo kwenye hatari kubwa kwa sababu wauzaji na wanunuzi wa vyakula hawajatilia maanani usafi wa bidhaa wanazouziwa.
Afisa huyo alisema yeyote ambaye atapatikana akiuza chakula bila kuwa na leseni iliyoidhinishwa na Wizara ya Afya atakamatwa.
“Wote ambao hawana kibali hicho kutoka katika Idara ya Afya wachukue leseni hiyo haraka kabla sheria haijawakabili,” alisema Akech.
Wito huu umetolewa siku kadhaa baada ya wakazi katika eneo hilo kulalamikia wahudumu wa vibanda ambao wanaonekana kutozingatia usafi wa vyakula wanapowauzia wateja wao.
Wakazi hao walisema jambo hilo limesababisha watoto wao kulazwa kwenye vituo vya afya kwa kusokotwa matumbo kwa kile kinachodaiwa kula vyakula hivyo.
Hata hivyo, miongoni mwa wauzaji hao walijitetea kwa kusema kuwa huwa wanajaribu ila bei ya bwelasuti jeupe la kujistiri huwa ghali mno ikizingatiwa kuwa wengi wao ni maskini.
Wameitaka wizara ya afya kuwapa nguo hizo kwa bei ya chini na ada ya kupata leseni kupunguzwa.