Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, Magharibi mwa Kenya, amesema tatizo la ugonjwa wa kipindupindu litadhibitiwa katika kaunti mbili za Nakuru na Baringo, iwapo wadau wote ikiwemo wanasiasa watakubali kuunga mkono mikakati ya kusaidia kudhibiti maradhi hayo.

Akizungumza siku ya Jumatano, mjini Mogotio, kwenye kikao cha dharura kujadili mkurupuko wa kipindupindu katika mpaka wa Nakuru na Baringo, John Ogange alisema hatua ya wanasiasa kufeli kuhudhuria kikao hicho ni dalili kwamba vita dhidi ya kipindupindu huenda vikakumbwa na vikwazo, iwapo wadau wa sekta ya afya wataamua kufunga biashara zinazochangia ugonjwa huo kuenea.

Huku takriban visa kumi vya kipindupindu vikidhibitishwa katika mpaka wa kaunti ya Nakuru na Baringo, daktari Mua Mbula wa Mogotio alisema wakazi wengi wa eneo hilo wamekataa kutii amri ya serikali kutumia vyoo wakati wa kwenda haja, na pia kuchemsha maji ya kunywa.

Mbula alisema umasikini umechangia hali hiyo, na pia biashara sugu ya pombe haramu ambayo hutengenezwa katika mazingira duni.

"Lazima tuungane pamoja kumaliza maradhi haya. Sio kwamba wanasiasa waogope kupoteza kura kwa kuunga mkono kufungwa kwa biashara ama serikali za kaunti kupoteza kodi," alisema Mbula.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Daktari mkuu wa Baringo Bw Kipsang Marachi na pia mkurugenzi wa afya ya umma kaunti ya Nakuru Dkt Joe Lenai.