Share news tips with us here at Hivisasa

Waendeshaji bodaboda mjini Kisii wameiomba serikali ya kaunti hiyo kuikarabati barabara ya kutoka mjini Kisii kuelekea eneo la Nyamataro.

Wito huo umetolewa baada ya barabara hiyo kuonekana kuwa mbovu zaidi na kushindwa kupitika hasa na waendeshaji pikipiki.

Akizungumza mjini Kisii hii leo, Jumatatu, mwenyekiti wa waendesha bodaboda hao katika kutuo cha uchumi Cyprian Mose na wahudumu wengine walimtaka gavana wa kaunti ya Kisii James ongwae kukarabati barabara hiyo ambayo imekuwa kero kwao.

Aidha, waendeshaji hao waliongezea kuwa wamekuwa wakifanya uchukuzi wao kwa muda mrefu wakitumia barabara nyingi ambazo ni mbovu kwa kaunti hiyo, na kusema kuwa huwa wanapata hasara kutokana na hali hiyo mbaya.

Kulingana na wahudumu hao, serikali imekawia kukarabati barabara hiyo ambayo iko mita mia moja kutoka ofisi ya Gavana Ongwae, na kila mara wanapouliza, hujibiwa kuwa barabara hiyo haiko chini ya serikali ya kaunti.

Kwa sasa wanamtaka mbunge wa eneo bunge la Kitutu Chache kusini Richard Onyonka kuwasaidia kuikarabati.

“Imekuwa ngumu kwetu kutumia pikipiki wiki mzima. Huwezi tumia pikipiki wiki mzima kabla haijaharibika kitu kinachohitaji pesa nyingi ili kuzirekebisha na pesa hizo hatuna,'” alihoji Moses Obiero mhudumu wa bodaboda.

Pia walidokeza kwamba sehemu nyingi za barabara za kaunti hiyo zilichimbuka na zina mashimo mengi na wanaitaka serikali kuingilia kati.