Waendesha bodaboda katika eneo bunge la Borabu, kaunti ya Nyamira wameomba serikali kuwahakikishia usalama wao.
Wito huo umetolewa baada ya wahudumu wawili kushambuliwa na majambazi wasiojulikana kwa siku tatu zilizopita kabla ya saa tatu usiku walipokuwa wanafanya shughuli zao za uchukuzi.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Kijauri, mwenyekiti wa wahudumu hao Francis Morara alisema wamekuwa wakishuhudia visa vya mashambulizi kila mara, na kuomba wahakikishiwe usalama wao kabla ya saa nne usiku wakati wengi wao wanafunga biashara zao za uchukuzi.
“Tunaomba tuweze kukumbukwa kama watu wengine kwa kuwekewa usalama wetu maana waendesha bodaboda wawili walishambuliwa na tunaendea kulalamikia jambo hilo hadi tuhakikishiwe usalama wetu,” alihoji Morara.
“Kama ni ushuru huwa tunatozwa, kwanini pesa hizo zisitumike kuwalipa maafisa wa polisi kushika doria kwa barabara za eneo hili hasa ile ya kutoka hapa Kijauri-Manga, na ile barabara ya kutoka Kijauri-Amakara na zinginezo? Aliongezea.
Kulingana na waendesha bodaboda hao, waliomwomba mbunge wa eneo hilo Ben Momanyi na serikali ya kaunti ya Nyamira kushirikiana kutengeneza barabara za eneo hilo ambazo nyingi hazipitiki.
Wakazi vilevile waliounga mkono ombi hilo, huku wakisema nao hawajahakikishiwa usalama wao kikamilifu kwani wizi wa ng’ombe na ujambazi kwa ujumla umeongezeka pakubwa katika eneo hilo.
“Tunaomba eneo bunge hili la Borabu usalama uwekwe kila upande ili nasi tuwe tunaishi kwa furaha na sio kwa kuogopa kila siku,” alisema Bearice Bosire, mkazi.