Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishena wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewaonya waendeshaji bodaboda na madereva wa magari ya aina ya probox dhidi ya kuendeleza biashara ya kusafirisha pombe haramu katika sehemu mbalimbali za kaunti hiyo.

Hii ni baada ya uchunguzi kubaini kuwa waendeshaji bodaboda pamoja na madereva wa magari hayo wanaendeleza biashara ya kusafirisha pombe hiyo katika kaunti ya Nyamira.

Akizungumza siku ya Jumatano na waandishi wa habari katika mji wa Nyamira kamishena huyo aliwataka machifu, manaibu wao pamoja na maafisa wa trafiki kuhakikisha usafirishaji huo umekomeshwa na kutoa tahathari kwa yeyote atakayepatikana kuwa atatiwa mbaroni na kushtakiwa.

“Naomba tuwakamate watu hawa. Maafisa wa trafiki na machifu muhakikishe kuwa hawa watu hawataendeleza biashara hiyo maana wengine wanatumia bodaboda, probox na ata matatu,” alisema Onunga.

Onunga alisema maafisa wengine katika kaunti zingine wamesimamishwa kazi kwa kutowajibikia kazi yao vilivyo huku akisema machifu pamoja na maafisa wa polisi wa kaunti hiyo ya Nyamira kama hawawezi kuwajibikia kazi yao kwa kupambana na pombe haramu huenda wakaachishwa kazi.

“Tutakagua kila sehemu haswa sehemu ambazo husimamiwa na machifu ili tuweze kubaini vita dhidi ya pombe haramu vimefika wapi. Atakayepatikana akishirikiana na wagema katika uuzaji wa pombe ataachishwa kazi maana tunahitaji machifu waliowajibika katika kazi yao,”aliongeza Onunga.