Share news tips with us here at Hivisasa

Wahudumu wa bodaboda katika mji wa Kisii wameombwa kulinda afya yao kwa kuvaa nguo nzito za kujikinga na baridi kali ya msimu huu wa mvua.

Akiongea siku ya Jumatatu na baadhi ya waendeshaji bodaboda katika mtaa wa Mwembe, mhudumu wa afya ya Jamii katika Kaunti ya Kisii Kepha King’oina aliwahimiza waendeshaji bodaboda kuwa kuna umuhimu wa kujikinga kutokana na baridi kali haswa msimu huu wa mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha katika jimbo la Kisii.

“Ni wajibu wa kila mtu kuwa na afya bora na ni lazima tujikinge na baridi kali ambayo huenda ikatuletea madhara katika miili yetu,” alisema King’oina.

Aidha, aliwaomba kuwa wangalifu wakati wamo barabarani kwa kuwa visa vingi vya ajali vimekuwa vikiripotiwa huku waendeshaji bodaboda wakiwa ndio wahusika wakuu.

“Nawaomba kuwa muwe waangalifu mnapokuwa barabani ili kujiepusha na ajali zinazoshuhudiwa katika mji huu wa Kisii ambazo nyinyi ndio wahusika wakuu,” aliongezea Kepha.

Kwingineko, aliwaomba kujiunga na wenzao katika vyama ili kujiendeleza kimaisha kwa kuanzisha miradi mbalimbali.

Kepha aliwaonya wanaodharau sekta ya bodaboda na kusema kuwa sekta hiyo imesaidia pakubwa kutoa ajira kwa watu wengi.