Wafanyabiashara katika soko kuu la Mogonga lililoko katika eneo bunge la Bomachoge Borabu wameitaka serikali ya kaunti ya Kisii kuwakarabatia soko hilo ambalo limeachwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa baada ya ukarabati huo kuanzwa na kuachiwa njiani.
Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko hilo siku ya Ijumaa jioni, mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo Benson Choti alisema kuwa soko hilo linapaswa kukamilishwa haraka iwezekanavyo ili kuwe na mpangilio na utaratibu wa kuwasilishwa bidhaa na kuondolewa kwa mazao humo ndani.
Alisema kuwa imekuwa vigumu kwa watu kuhudumu katika soko, hasa siku ya Jumapili ambayo ndio siku kuu teule ya shughuli za biashara, ambapoa alisema kuwa wengi wa wafanyabiashara wamekuwa wakipanga bidhaa zao za kuuza hadi barabarani, hali ambayo inasababisha njia kufungwa na kuleta msongamano wa magari.
Alishangaa ni kwa nini imechukua zaidi ya miaka mitatu tangu awamu ya kwanza ya ukarabati huo, kuasisiwa na kuachiwa njiani miezi mitatu tu.
Choti alishauri serikali ya kaunti kutafuta njia mbadala ya kuwapangilia wafanyabiashara hao ambao wengine wao wamekuwa na shida na baadhi ya watoza ushuru ambao wamekuwa wakiwahamisha kutoka maeneo wanamofanyia biashara zao.
Mwenyekiti huyo vile vile aliitaka serikali ya gavana Ongwae kuzuru soko hilo hasa siku kuu ya biashara ambayo huwa kila Jumapili na kujionea matatizo ambayo wanapitia wanapotekeleza shughuli zao za biashara.