Wafanyabiashara katika katikati mwa mji wa Kisii wameiomba serikali ya Kaunti ya Kisii kupitia Idara ya Biashara, ile ya Mpangilio wa mji pamoja na Ardhi kuwajengea ua wa kudumu.
Akiongea siku ya Jumapili, mmoja wa wanakamati wa wasimamizi wa soko hilo Samuel Mosioma alizitaka wizara husika kuharakisha kuweka ua huo ili kuepusha baadhi ya wenye magari ambao wamekuwa wakiyaegesha magari yao kiholela na wakati mwingi kuwafungua njia na kuwa vigumu kwa wafanyibiashara hao kusafirisha bidhaa zao kuenda ndani ya vibanda vyao.
Mosioma alitaja kisa ambacho mmoja wa wamiliki wa magari hayo ya kibinafsi wiki jana kidogo amgonge mama mboga mmoja baada ya gari lake kupotoka barabarani na kutokomea hadi eneo wanalouuzia bidhaa zao na kumtaka idara ya biashara washirikiane na ile ya mipangilio ya mji kuwatengezea soko hilo kwa kujenga ua ambao utawakinga kutokana na magari hayo.
Kwingineko, baadhi ya wafanyibiashara hao wakiongea Jumapili hiyo katika eneo hilo la kufanyia biashara wakiongozwa na Bi Jane Kemuma, walisema soko hilo limeachwa nyuma kwa sababu ya mzozo uliotokea mwisho wa mwaka jana ambapo waliandamana kitu ambacho kimechelewesha ukarabati wake.
Hata hivyo kiongozi Mosioma alisema wanatarajia kuwa mkutano ambao wanapanga kufanya mwezi ujao na baadhi ya maafisa wa kaunti hiyo ya Kisii utazaa matunda na kuongezea kuwa suala hilo litakuwa katika ajenda yao ya kujadiliwa ili kupata suluhu ya suala hilo.