Wafanyibiashara wa kuuza maziwa mjini Kisii walifikishwa katika mahakama ya Kisii siku ya Jumatano na kushtakiwa kwa kutofuata na kuzingatia sheria za afya.
Wafanyibiashara hao sita walitiwa mbaroni walipopatikana wakiuzia maziwa mahala palipo pachafu huku wengine wakiongeza maji na unga wa ngano kwa maziwa jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Shughuli hiyo ya kuwatia mbaroni wafanyibiashara hao iliendeshwa na msimamizi wa sheria za maziwa mkoani Nyanza David Wakungu siku ya Jumatano.
Wasita hao walifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kukiuka sheria zilizowekwa kwa uuzaji wa maziwa hayo.
Washukiwa hao waliachiliwa baada ya kulipa dhamana ya Sh1,500 kila mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kisii, Wakungu aliyeendesha shughuli hiyo alisema washukiwa hao hawazingatii sheria za kuuza maziwa nchini.
“Tuliwatia mbaroni wafanyibiashara hao kwa makosa ya kuuzia maziwa maeneo yaliyo chafu, kuongeza maji kwa maziwa pamoja na kuongeza unga wa ngano. Hiyo ni kudhulumu afya ya binadam,” alisema Wakungu.
Msimamzi huyo aliapa kuendelea na shughuli hiyo ya uchunguzi wa kutambua wengine amabao wanatekeleza vitendo sawia na vya waliotiwa mbaroni.
Aliwaomba wafanyibiashara wa maziwa kujali afya ya binadamu wanapoendeleza biashara yao.